​WCF KINARA MAONESHO YA NANENANE 2019

News Image

Imewekwa: 30th Nov, -0001

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), umeibuka mshindi wa kwanza katika Maonesho ya 27 ya Wakulima (Nanenane) yaliyofanyika kuanzia tarehe 28 Julai hadi 8 Agosti katika viwanja vya Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Mgeni Rasmi, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) kwenye kilele cha maonesho hayo, Bw. Anselim Peter Mkurugenzi wa Uendeshaji wa Mfuko amesema WCF imekuwa Mshindi wa Kwanza katika kundi la Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kutokana na uboreshwaji wa huduma zinazotolewa kupitia mtandao jambo ambalo limerahisisha upatikanaji wa huduma kwa wadau wake.

Bw. Peter amesema sambamba na ushindi huo, WCF itaendelea kuboresha huduma zake ikiwemo kufungua ofisi zaidi mikoani ili kuwafikia wadau wengi zaidi. Aidha, ili kurahisisha upatikanaji wa huduma na kuongeza ufanisi zaidi, Mfuko umewekeza katika matumizi ya teknolojia na kwa sasa upo katika hatua za mwisho za kuzindua Mfumo wa Kuwasilisha Madai kwa njia ya Mtandao, aliongeza Bw. Peter.

Akizungumzia madhumuni ya ushiriki wa maonesho ya Nanenane, Bw. Peter amesema lengo la WCF kushiriki kwenye maonesho ya Nanenane ni kuunga mkono kwa vitendo juhudi za Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Dkt. John Pombe Magufuli katika kuhakikisha huduma za Serikali zinawafikia wananchi kwa urahisi na kwa wakati. Alihitimisha kuwa WCF imetumia fursa hii kupata mrejesho wa moja kwa moja kutoka kwa wadau wake pamoja na kutoa elimu kwa waajiri, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla kuhusu Mfuko ikiwa ni pamoja na taratibu za kuwasilisha madai iwapo mfanyakazi atapata ajali, ugonjwa au kifo kutokana na kazi.

Alifafanua kuwa katika maonesho hayo ya Nanenane walitembelewa na baadhi ya wanufaika wa huduma za Mfuko ambao walitoa ushuhuda wa namna walivyohudumiwa na kupata Mafao yao kwa wakati. “Binafsi nimefarijika sana kusikia kutoka kwa wafanyakazi waliowahi kulipwa fidia wakishuhudia ubora wa huduma zetu na namna walivyopokea mafao yao kwa wakati”, alisema Bw. Peter.

Awali Waziri Mkuu alizipongeza Taasisi zote zilizopata ushindi kwenye maonesho hayo ambapo pia alipata fursa ya kutembeleana kukagua baadhi ya mabanda. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Nanenane kwa mwaka huu ilikuwa, “Kilimo, Mifugo na Uvuvi kwa Ukuaji wa Uchumi wa Nchi.”

Maonesho hayo yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali akiwemo Katibu Mkuu wa CCM Dkt. Bashiru Ally, Waziri wa Ulinzi Mhe. Dkt. Hussein Mwinyi, Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Luhanga Mpina, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Nchi OR - TAMISEMI, Mhe. Josephat Kandege na Naibu Waziri wa Madini Mhe. Stansalaus Nyongo.