Maonesho ya Viwanda Mkoa wa Pwani

News Image

Imewekwa: 30th Nov, -0001

MAKAMU wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan, amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), kuendelea kuwabana waajiri ambao bado hawajajisajili na hawawasilishi michango katika Mfuko huo.

Makamu wa Rais alitoa wito huo leo Oktoba 29, 2018 alipotembelea banda la Mfuko huo kwenye maonesho ya viwanda Mkoa wa Pwani kwenye viwanja vya CCM-Sabasaba, Picha ya Ndege Mkoani Pwani.

Alisema viwanda vimeongezeka nchini na kwamba huduma za WCF zitahitajika sana kwa wakati huu na hivyo kuutaka uongozi wa Mfuko, kuhakikisha unaendelea na ufuatiliaji kwa waajiri ambao bado hawajajisajili na hawawasilishi michango katika Mfuko. Waajiri watekeleze takwa hilo la kisheria ili mfanyakazi anapoumia aweze kupata haki yake ya fidia.

“Waajiri wao muwabane wajisajili na mfuko na waweze kuwasilisha michango ili Mfuko uendelee kuwa na uwezo wa kulipa fidia, pale watoto wetu (wafanyakazi) wanapokatika vidole au kuumia waweze kupata haki zao.” Alisisitiza.

Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi unashiriki maonesho hayo ya viwanda yanayofanyika kwa mara ya kwanza katika Mkoa wa Pwani na waajiri, wafanyakazi na wananchi wamekuwa wakipita kwenye banda la Mfuko huo kupata elimu kuhusu shughuli za Mfuko.

Katika hatua nyingine, WCF imekuwa miongoni mwa taasisi zilizotunukiwa vyeti vya shukrani kwa kuwezesha maonesho hayo. Katika hatua ya kuimarisha Hifadhi ya Jamii, Tanzania, Serikali ilianzisha Mfuko wa Fidia Kwa Wafanyakazi kwa mujibu wa kifungu cha 5 cha Sheria ya Fidia kwa Wafanyakazi, Sura ya 263 kilichofanyiwa marejeo mwaka 2015 ili kuhakikisha kila mfanyakazi Tanzania Bara kutoka sekta ya umma na binafsi anapata fursa ya kuwekewa kinga na mwajiri wake ili anapopata majeraha au magonjwa awapo kazini basi aweze kufidiwa kwa mujibu wa sheria.